Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This


Hellen George ‘Ruby’.
NINAZIDI kumshukuru Mungu kwa kila jambo katika mwaka huu. Kuna waliotamani kuiona siku hii, lakini hawakupata nafasi hiyo. Ila mimi na wewe bado tunaendelea kupumua kwa kudra za Mwenyezi Mungu.


Barua yangu nzito leo imuendee mdogo wangu, mwenye sauti nzuri na mwanana, Hellen George ‘Ruby’ ambaye ninakumbuka mwishoni mwa mwaka 2017 aliahidi kuanza rasmi kazi yake ya muziki Mwaka Mpya wa 2018.

Kilichonishtua na kunishangaza hadi kuamua kumuandikia waraka huu Ruby ni kutokana na kusambaa kwa haraka zaidi kwa picha zake zikimuonesha sehemu za nyuma akiwa amefungashia kinyume na mwonekano wake ambao kila mtu anaufahamu.

Kubadilika kwa mtu kunaweza kutokea hata kwa siku moja, lakini mkanganyiko uliopo katika picha hizo ndiyo hasa ulionihamasisha kumuandikia Barua Nzito mdogo wangu, Ruby.

Sijawahi kuchukizwa na wimbo wako hata mmoja, ninamaanisha mimi ni shabiki wako wa damu, ninapenda sauti yako uliyojaliwa na Mwenyezi Mungu. Ninapenda uwezo wako wa kuimba na kuchezea sauti yako unavyotaka wewe. Hongera kwa hilo!

Kwa nini Ruby unaiga kasumba ya baadhi ya mastaa kupiga picha na kuposti huku wakiwa na makalio feki au kigodoro? Ama ya kuchonga, kutumia dawa za Kichina au kufanya editing.
Sikujua nini dhamira yako, unaonesha unahitaji kuwa na umbo la namna hiyo au unamkosoa Mungu kwa namna alivyokuumba?

Hivi Ruby ni kweli unatamani kuwa bonge au kuwa na makalio makubwa au ni watoto wa mjini wameungaunga picha na kuziposti mtandaoni? Lakini kama zimeungwa na watu baki mbona hata kwenye akaunti yako ya Instagram nawe umeziposti?

Nashawishika kusema kuwa kwa namna yoyote ya hizo picha, hata wewe unahusika, iwe kwa kuweka kigodoro, kupaka dawa za Mchina au ‘kuediti’.
Wakati mwingine Mungu huwa ana kusudi lake na inawezekana alikupa umbo zuri ulilonalo na akakuongezea sauti nzuri ya kumtoa nyoka pangoni. Vipi kama leo hii Mungu akakubadilisha kwa kukupa mwili wenye makalio makubwa halafu akaiondoa sauti tamu uliyonayo? Si utaanza kulalamika na kuona Mungu hakukutendea haki?

Ruby mdogo wangu, kama mwonekano wako mpya kwa mwaka 2018 ni huo, ni sawa, lakini uwe ni mwonekano wa halisi, lakini kama umechoma sindano, umekula dawa za Mchina au umefanya editing unakuwa unakosea sana!

Yawezekana dada yangu mapenzi yanakuendesha, pengine umempata jamaa ambaye amekuwa akikuumiza kwa kuwasifiwa na kuwashobokea wanawake wenye maumbo makubwa? Yamkini na wewe ukaamua kufanya ulichofanya ili kumridhisha mpenzi wako, kama ni kweli huyo hakupendi, huo ni utumwa wa kimapenzi.

Mwanaume wa namna hiyo hakufai kabisa, mtu anayekupenda kwa dhati, huwa haangalii una kasoro gani, anachokifanya ni kukupenda wewe kama Hellen na si wewe kama Ruby.
Sitaki kukulaumu moja kwa moja wewe, inawezekana kuna mtu ambaye amefanya mchezo wa kuediti hizo picha bila ridhaa yako, basi una kila sababu ya kumshtaki kwa sababu amezua sintofahamu na nina hakika kuna watu ambao wamekuponda, wamekutukana, wamekukejeli na mambo mengine kama hayo.

Lakini, hata hivyo, kama ni figa ambayo imefumuka kwa sababu ya unene ni vyema ukajitokeza na kuwapa ukweli mashabiki wako ili ambao wamekuwa wakikuponda uwakate kabisa kilimilimi.
Nimalizie kwa kusema kuwa, mdogo wangu, Ruby ridhika na vile ulivyoumbwa, kwani kuna watu wana miili mikubwa na wanatamani sauti yako, lakini kamwe hawawezi kuipata kwa sababu Mungu humgawia kila mtu kipawa chake.

Post a Comment

 
Top