Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Mwanamitindo wa Bongo, Hamisa Mobeto.
Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na kuuona mwaka mpya 2018. Kuna ndugu, jamaa na marafiki wengi ambao walitamani kuuona mwaka mpya lakini Mungu aliwapenda zaidi. Wengine wako vitandani hospitalini, lakini mimi na wewe tumeweza kusherehekea Krismasi na Mwaka Mpya kwa shangwe.

Leo kwenye Barua Nzito, ninapenda kumkumbusha dada yangu kipenzi ambaye ni Mwanamitindo wa Bongo, Hamisa Mobeto. Dada yangu, nafasi uliyonayo kwenye jamii ni kubwa. Ni nafasi ambayo imekufanya utambulike ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kwa kazi na figisufigisu zako za kila siku.
Kupitia shughuli zako za kila siku, umeweza kupata dili mbalimbali ambazo kama ukizitumia vizuri zinaweza kukufanya ukatoboa mazima kwa kuwa na maisha f’lani hivi mazuri.
Ikiwa tumeuanza mwaka mpya 2018, ninapenda kukuasa dada yangu Mobeto, inawezekana hatujuani ana kwa ana kwa sababu sikumbuki kama nimeshawahi kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na wewe. Lakini najaribu kukufikishia barua yangu kwa sababu ya mapenzi mema kwako na kwa kukutakia heri ya mwaka mpya.
Mobeto, ninakukubali kwa maana ya kazi yako ya u-modo lakini pia kwa jinsi unavyojua kupangilia mavazi yako, hujawahi kuharibu.
Leo ninajaribu kukukumbusha kuwa, mwaka jana ulitengeneza sana vichwa vya habari mbalimbali kutokana na mishe zako za kila siku.
Ninachoamini mimi kwa mwaka jana ulitengeneza mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi. Kama kweli mtandao wako utautumia vizuri basi una nafasi kubwa ya kutoboa kwa kwenda levo za kimataifa.
Kitendo chako cha kupata shavu la kupata shoo nchini Uganda inamaanisha kuwa unakubalika bila kujali upinzani na figisu za aina yoyote iliyokuwepo kwenye shoo hiyo.
Nakumbuka Novemba 4, mwaka jana ulikuwa ni mmoja wa wanamitindo wa Kitanzania ukiwakilisha na Afrika Mashariki uliyechanguliwa kwenye Tuzo ya Starqt Awards zinazohusisha biashara, mitindo, burudani na ukachaguliwa katika vipengele vya ‘People Choice Awards’ na ‘Super Mum’ ila amefanikiwa kuibuka kidedea katika kipengele kimoja tu. Tuzo ambazo zilitolewa katika Ukumbi wa Bedford View City Hall, mjini Johannesburg Afrika Kusini.
Umekuwa na sarakasi za hapa na pale kwenye maisha yako lakini kama ukizitumia vizuri basi zinaweza kukusaidia kufika sehemu nzuri.
Kama msanii kuna wakati unakuwa uko kwenye ‘peak’ kila mitandao inakusema wewe, vyombo vya habari mbalimbali navyo vinaandika habari zako. Huo ndiyo muda muafaka wa wewe kufanya biashara kama ukishindwa kuutumia vyema muda huo ambao uko juu basi utakuwa umefeli.
Wapo wasanii wengi ambao walipata nafasi kama ya kwako lakini pengine kwa kuwa na akili ya ziada, hawakuwa na washauri wazuri au sikupata nafasi ya kuwakumbusha kwenye barua yangu. Wakajikuta wametumia vibaya pesa, rasilimali na muda wao pasipo kunufaika na ustaa wao.
Mobeto kwa kila unachofanya lazima ujue kuwa wewe ni mama wa watoto wawili ambao unatakiwa kuwalea katika mazingira na maadili mzuri hasa ya Kitanzania.
Fanya jambo kwa kuangalia pia je, ni alama au athari zipi unaweza kuziacha kwa wanao baada ya maisha yako ya u-modo.
Mwisho kabisa, napenda niwatakie kila la heri wasomaji wa Barua Nzito kwa mwaka huu 2018. Mungu akusimamie na akupe wepesi katika kila jambo jema unalolifanya katika maisha yako ya kila siku.

Post a Comment

 
Top