Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatekeleza sera mbali mbali zenye muelekeo wa kupunguza umasikini.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa Ufunguzi wa Soko jipya la kisasa lililopo Konde, wilaya ya Micheweni, Pemba.
Makamu wa Rais alisema Sekta ya kilimo inatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 70 na inachangia kiasi cha asilimia 50 ya chakula kinacholiwa Zanzibar, hivyo ni jukumu la Serikali kuweka mazingira bora kwa wananchi ili waweze kujiletea maendeleo.
“Soko hili la kisasa litapelekea kuongezeka kwa ajira, kupitia kuongezeka kwa shughuli za kibiashara na kilimo, kuongezeka kwa uzalishaji, na uongezaji thamani wa mazao, hata kuongezeka kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla”.
Makamu wa Rais alisema ni dhahiri kwamba kuondoka na umasikini kutategemea sana mafanikio ya shughuli zinazotekelezwa katika sekta ya kilimo “hivyo ni vyema tukaboresha kilimo kwa kubuni fursa zaidi na kuongeza kipato kwa wananchi wetu”.
Makamu wa Rais alitoa wito kwa uongozi wa Shehia, halmashauri, Wilaya na mkoa kuhakikisha kuwa soko linasimamiwa kwa ukaribu na linatumiwa kwa kuzingatia taratibu zitakazohakikisha uendelevu wa huduma zitakazotolewa na kuona malengo yaliokusudiwa yanafanikiwa ikiwamo kuwaletea wananchi mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
Aidha Makamu wa Rais aliwataka wananchi kuendelea kuwa kitu kimoja katika kulienzi soko ili liweze kuboresha maisha yao na ya vizazi vijavyo.

Post a Comment

 
Top