Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) akiongozwa na Meneja wa shamba la Miti Kawetire, Arnorld Shoo kukagua moja ya eneo katika shamba hilo ilipopita barabara ya lami ambayo ipo juu zaidi ya nyingine nchini ikiwa na urefu (Altitude) wa mita 2961 kutoka usawa wa bahari wakati wa zaira yake ya kikazi jana mkoani Mbeya. Alisema Serikali itaboresha mazingira ya eneo hilo ili yatumike kama kivutio cha utalii nchini.
Bofya kitufe cha PLAY kuangalia VIDEO

Na Hamza Temba, Mbeya
………………………………………………..
Serikali imesema
itaboresha mazingira ya kivutio cha utalii cha barabara ya lami ambayo ipo juu
zaidi kutoka usawa wa bahari kuliko barabara zote nchini ili kupanua wigo wa
vivutio vya utalii na kuongeza idadi ya watalii na mapato.

Hayo yameelezwa jana na
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga baada ya kutembelea shamba
la miti la Kawetire wilayani Mbeya na kujionea sehemu ya barabara ya lami
inayopita katikati ya shamba hilo katika mlima Kawetire kwenye safu za milima
ya Mbeya.

Eneo hilo la barabara hiyo
ambayo hupitisha magari kutoka Jijini Mbeya kwenda katika Wilaya ya Chunya na
Mikoa ya Singida na Tabora lina urefu (Altitude) wa mita 2961 kutoka usawa wa
bahari katika Latitude 08’ 35 S na Longitude 33’ 25 E.

“Hatutaki ule utalii
wa kutegemea wanyamapori pekee, hii sasa ni sehemu ya aina nyingine ya utalii
ambayo ni lazima tuiboreshe tuweke kibao kizuri tuweke mazingira mazuri pamoja
na kukitangaza ili watanzania na watalii kutoka nje waweze kutembelea hapa,”
alisema Hasunga.

Alisema ili kufikia
lengo liliwekwa na Serikali la kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni mbili
mwaka 2020 na milioni 8 mwaka 2025 vivutio vyote vya utalii vilivyopo nchini
vitatambuliwa, kuimarishwa na kuviwekea miundombinu itakayowavutia watalii
kuvitembelea.

Aidha aliuagiza
uongozi wa shamba hilo kushirikiana na wakala wa huduma za barabara –Tanroads
katika kuboresha mazingira yanayozunguka eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuweka
bango la kisasa la kutambulisha eneo hilo, kujenga bustani na maeneo rafiki ya
kupumzikia kwa ajili ya kuwavutia watalii kutembelea eneo hilo na kupiga picha.

Mbali na kivutio hicho
aliuagiza uongozi wa shamba hilo kutobomoa majengo ya kale yaliyotumiwa na
wakoloni katika shamba hilo na badala yake yatumike kwenye utalii wa mambo ya
kale sambamba na utalii wa misitu ya kupandwa inayopatikana pia katika shamba
hilo.

Hata hivyo alisema
kupitia mradi wa REGROW wa kuendeleza utalii kanda ya kusini Serikali imepokea
mkopo wa masharti nafuu wa dola za Kimarekani milioni 150 sawa za zaidi ya
bilioni 340 za kitanzania kutoka benki ya dunia kwa ajili ya kusaidia kuboresha
miundombinu ya vivutio vya ukanda huo.

Kwa upande wake Meneja
wa shamba hilo, Arnorld Shoo alisema eneo hilo la barabara limekuwa ni kivutio
cha kipekee cha utalii katika shamba hilo ambapo pia hupata mapato kupitia watu
na vikundi mbalimbali ikiwemo wanakwaya na wanafunzi ambao hufika eneo hilo kwa
ajili ya kupiga picha za kumbukumbu.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (kulia) na Meneja wa shamba la Miti Kawetire, Arnorld Shoo wakiangalia bango linaloonesha eneo katika shamba hilo ilipopita barabara ya lami ambayo ipo juu zaidi ya nyingine nchini ikiwa na urefu (Altitude) wa mita 2961 kutoka usawa wa bahari wakati wa zaira yake ya kikazi jana mkoani Mbeya. Alisema Serikali itaboresha mazingira ya eneo hilo ili yatumike kama kivutio cha utalii nchini.

Post a Comment

 
Top