Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameshauri kutazamwa mchakato mzima wa ubinafsishaji kwa kufanya ukaguzi maalumu wa sera ili kutoa mapendekezo ya kurekebisha makosa yaliyofanyika.

Mh. Zitto katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii leo amesema Serikali inaweza kuunda tume kutazama namna ubinafsishaji ulivyofanyika na kuchukua hatua.
Kusinyaa kwa ukuaji wa Uchumi wetu na Jambo la Kampuni ya Airtel
Ninasimama na uchambuzi niliyoufanya na kupitishwa na Kamati Kuu ya Chama chetu cha Act Wazalendo kuwa ukuaji wa Uchumi wa nchi yetu unasinyaa. Uchambuzi wa takwimu zilizotolewa na NBS hauwezi kuwa kosa kwa namna yeyote ile. Sera za Uchumi za Serikali ya Awamu ya zilizopelekea kuanguka kwa mikopo kwenda sekta binafsi na hivyo ugavi wa fedha ( money supply M3 ) zimesababisha ukuaji wa Uchumi wa nchi yetu kusinyaa. Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wamethibitisha hilo kwenye Taarifa yao na wameagiza Serikali kutazama upya vyanzo vyao vya Takwimu. Rais John Pombe Magufuli hawezi kuzuia uchambuzi huru wa kisera na pia takwimu za Serikali zinakosoleka na tutaendelea kutoa takwimu mbadala pale NBS wanapotoa Takwimu za uongo kufurahisha watawala.
Jambo la Airtel ni kama NBC
Nimejizuia kulisemea jambo hili Kwa sababu mbalimbali. Sababu kubwa ni kwamba unahitaji MAARIFA kushughulika na masuala kama haya.
Tukiwa PAC tulifanyia kazi sana suala la Sera ya Ubinafsishaji. Katika kila Taarifa yetu ya Mwaka tulikuwa na sehemu maalumu iliyoeleza ufuatiliaji wetu wa utekelezaji wa Sera ya ubinafsishaji. Ubinafsishaji wa TTCL ni suala tulilitolea Taarifa mara kadhaa Bungeni na Taarifa yetu ya mwisho ilikuwa January 2015. Ni ukweli usio na mashaka kuwa Kampuni ya Celtel ( sasa Airtel ) haikulipa chochote kuwezesha kumiliki hisa kwenye Celtel Tanzania na pia uuzwaji wa Celtel kwenda Zain na kisha Airtel ulipelekea Tanzania kupoteza Mapato ya Kodi ya ongezeko la Mtaji ( capital gains tax ). Mwaka 2011 Mzee Harry Kitilya akiwa Kamishna Mkuu wa TRA alituletea kwenye Kamati uchambuzi wa mapato tuliyopoteza ya jumla ya USD 312m kwa mauzo ya Zain kwenda Airtel. Kazi ndio iliwezesha kufanikiwa kutunga sheria ya capital gains tax mwaka 2012 na kuziba mwanya huo wa makampuni ya Kimataifa kukwepa kodi nchini kwetu.
Hata hivyo tunahitaji kushughulika na jambo hili la Airtel kwa muktadha wa zoezi zima la Ubinafsishaji nchini. PAC iliagiza CAG kufanya Post privatization audit ya Mashirika kadhaa ikiwemo Benki ya NBC. Matokeo yake tuliyawasilisha Bungeni. Uuzwaji wa NBC nao ulikuwa ni wa bure na huwezi kushughulika na kampuni moja moja bila kutazama muktadha mzima wa zoezi la Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma.
Ushauri wangu ni kutazama mchakato mzima wa Ubinafsishaji kwa kufanya ukaguzi maalumu wa sera nzima ili kutoa mapendekezo ya kurekebisha makosa yaliyofanyika. Hii itawezesha nchi kutoyumbayumba na matukio na badala yake kuwa na ‘ policy consistency ‘ kwenye jambo zima la Ubinafsishaji. Rais anaweza kuunda Tume ya Rais ( commission of inquiry) kutazama namna ubinafsishaji ulifanyika na kuchukua hatua za kisayansi baada ya matokeo ya kazi hiyo. Hili la Airtel linaweza kushughulikiwa humo na kupata matunda mazuri zaidi.
Heri ya Mwaka Mpya 2018. Mola awabariki sana na kumaliza salama mwaka 2017

Post a Comment

 
Top