Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
 
MWENYEKITI mpya wa Umoja Wanawake Tanzania (UWT)Taifa,Gaudentia Kabaka ,ameitaka jumuiya hiyo kuanzia ngazi ya chini kuongeza wanachama wapya kwani ndio mtaji wa chama na jumuiya zake.
Aidha amepokea wanachama wapya 750 wa UWT mkoani Pwani wakati alipopokelewa mjini Kibaha baada ya kupata ushindi wa kuongoza nafasi hiyo .
Mwenyekiti huyo alipokea wanachama hao ,mjini humo na kusema wameingia wakati muafaka wakati chama na serikali ya awamu ya Tano ikifanya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na maendeleo.
Aliwataka wanaCCM kuanza maandalizi ya kuhakikisha chama na jumuiya zina uhai kwa wanachama wapya na kulipia kadi, ili kuimarisha nguvu ya CCM kabla kuingia kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Gaudentia alisema UWT imejipanga  kuingiza wanachama wapya na kuwalea na kuwawezesha kwa fursa za masoko ili kujiimarisha kiuchumi na kuwa na uhakika katika kujenga jumuiya imara.
Alisema kwa sasa kila kata ,wilaya na mkoa kazi iliyoko mbele yao ni kufanya kazi kwa bidii na maarifa ikiwemo kuongeza mtaji wa wanachama wapya kwa kuwa ndio mtaji wa kisiasa.
Gaudentia ,alisema mwisho wa uchaguzi ndio mwanzo wa uchaguzi mwingine wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.
Aliwataka makatibu wa UWT kujitathmini kwa majukumu yao ya kazi kwa kufuatilia maendeleo yanayofanywa na serikali, ili kuwa rahisi kuieleza jamii yanayotekelezwa kwa takwimu sahihi.
“Ni wakati wa viongozi wa jumuiya kutoka ofisini ,nendeni mkajue yanayoendelea kwenye elimu, afya nishati ,msiogope tokeni mkafuatilie muwe na lakuwaeleza wananchi,” alisema Gaudentia.
Gaudentia alisema ,wasimuone ameanza kuwa mkali ila ni lazima kwenda na kasi ya Rais Dk. John Magufuli, ambaye wakati wote anafanya kazi ya kuijenga Tanzania mpya.
“Mbali na miradi ya kiuchumi iliyopo makatibu wa ngazi mbali mbali tafuteni takwimu sahihi zinazohusu masuala ya huduma za kijamii hasa zinazowahusu wanawake.” alisema Mwenyekiti huyo.
Gaudentia ,alisema  UWT kupitia uongozi huo mpya  ni lazima irejeshe heshima yake ya kuwa chombo cha kuwaunganisha wanawake  wa mijini na vijijini ili wapate maendeleo.
Aliwashukuru wajumbe wa mkutano kuu wa tisa wa umoja huo kwa kumuamini kisha kumchagua kwa kura nyingi .
“Natoa ahadi yangu tena kwenu kwamba mmeniamini nami nitatenda mema kwenu kwa kurejesha matumaini ya kutenda na kusimamia maendeleo ya wanawake,”
Akizungumza kabla ya mwenyekiti ,Katibu Mkuu wa UWT Taifa Amina Makilagi, alisema lengo la kufika Wilaya ya Kibaha ni kusalimiana na kufahamiana na wanachama na viongozi wa jumuiya ya wanawake wilayani Kibaha na Mkoa kijumla.
Alisema  kwamba jumuiya hiyo itembee kifua mbele,imelamba dume kwani wamempata kiongozi jembe na mchapakazi.
“CCM haifanyi makosa ,haichagui wala kuteua viongozi barabarani ,na mama Gaudencia Kabaka amepitia nafasi mbalimbali za serikali na chama hivyo hana mashaka nae” alisema Makilagi .
Kwa upande wake ,Naibu Waziri wa Nishati ambae pia ni Mbunge wa viti maalumu mkoani Pwani ,Subira Mgalu alimhakikishia mwenyekiti Gaudentia kuwa atashirikiana na uongozi huo mpya kuboresha maisha ya wanawake kwenye upande wa nishati .
“Nishati ikipatikana ya uhakika wanawake hawatalala kwa kutumia vibatari ,watapata umeme pia kwenye zahanati na kujifungua bila shaka ya kukosekana nishati ya uhakika,” alisema Mgalu.
Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thwayiba Kisasi, alisema dhamira ya UWT ni kuzitatua changamoto mbali mbali zinazowakabili akina mama ili wanufaike na matunda ya kuwa mwanachama wa Umoja huo.
Alisema kwamba viongozi hao hawatowaangusha kiutendaji bali watatumia uzoefu na taaluma zao kuleta maendeleo endelevu ndani UWT.
Awali mwenyekiti wa UWT mkoani Pwani Farida Mgomi , alisema mkoa huo umepokea kwa Furaha ushindi wa viongozi Taifa na katika kuthibitisha hilo ndio maana amepokea umati wa wanachama hao wapya.
Pia alimkabidhi mwenyekiti wa UWT Taifa na makamu wake zawadi mbalimbali ikiwemo mkeka,kanga,vitenge,seti ya vyombo vya chakula,msala wa ibada na kikoi.

Post a Comment

 
Top