Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Rais Magufuli akisalimiana na Msanii Mrisho Mpoto.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Mgufuli anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’ itakayozinduliwa Ijumaa, Disemba 8, mwaka huu kupitia ‘Usiku Wa Kitendawili’ mjini Dodoma huku Kikundi cha Sanaa cha Mpoto Theatre Gallery cha Mrisho Mpoto kikitoa burudani.
Kampeni ya Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’ itaratibiwa na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Msanii wa Muziki wa Asili Tanzania, Mrisho Mpoto kupitia Kikundi chake na wadau wa sanaa za ubunifu ndiyo watasherehesha kwa burudani katika usiku huo wa Kitendawili.
Akiongea na wadau wa sanaa katika maandalizi ya kampeni hiyo ya kitaifa itayokuwa ikifanyika kila mwaka sambamba na maadhimisho ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julis Kambarage Nyerere, Mrisho Mpoto amesema, kampeni hiyo ina lengo la kurejesha hali ya Uzalendo na Utaifa katika kutatua changamoto zilizojitokeza na zitakazojitokeza ndani ya taifa letu.
Mambo yatakayozungumza kwenye usiku huo ni kudhibiti na kukomesha mmomonyoko wa maadili kwa viongozi wa umma, kuongezeka kwa tuhuma za rushwa, kuibuka kwa ufisadi, ubadhilifu wa mali za umma na kuongeza hali ya kufanya kazi na Uzalendo.
“Usiku wa Kitendawili utatumika kama jukwaa la kuwaleta pamoja Watanzania na viongozi wao ili kukumbushana kuhusu wajibu na kujadili mustakabali wa taifa. Kutakuwa na vivutio mbalimbali na wimbo maalumu kutoka kwa wasanii maalumu,” alisema Mpoto.
”Tunataka kuunadi Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’ kwa sababu tunaamini Uzalendo na Utaifa lazima uwepo ili kufanikisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kuunga mkono juhudi za Rais, Dkt. Magufuli, za kujenga Taifa lenye Uzalendo, Utu, Weledi na Uadilifu uliotukuka. Nimejitoa toka mwanzoni mwa harakati hizi na hata nyimbo zangu zinazungumzia kuwaunganisha wanajamii wa Kitanzania wapatao 120.
Mpoto aliongeza kuwa, lengo kuu la maadhimisho hayo kuambatana na maadhimisho ya kifo cha Baba wa Taifa kuanzia mwaka 2018 ni kutumia jukwaa hilo kufikisha ujumbe wa umuhimu wa kujenga na kuendeleza Utaifa.
Baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo kufanyika mjini Dodoma, pia itafanyika kwenye mikoa yote nchini na itasimamiwa na Kamati za Utamaduni za mkoa na wilaya.Usiku wa Kitendawili ulianzishwa baada ya Mpoto kuachia Wimbo wa ‘Kitendawili’ na baadaye kufikiria kuanzisha usiku wa wimbo huo na kuanzisha mjadala kuhusu uzalendo.

Na Mwandishi Wetu/GPL

Post a Comment

 
Top