Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Salum Njwete ‘Scorpion’ alipokuwa akipelekwa mahakamani leo.
SALUM NJWETE maarufu kama Scorpion anayetuhumiwa kumtoboa macho Said Mrisho, jana alianza kujitetea katika kesi inayomkabili kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kuhusu kumjeruhi na kumtoboa macho kinyozi Said Mrisho, kumuibia cheni zake na pesa.

Scorpion alianza kujitetea kwenye kesi hiyo baada ya mashahidi wa pande zote kumaliza kutoa ushahidi wao na mahakama kumkuta na kesi ya kujibu.
Katika utetezi uliochukua zaidi ya saa mbili alianza kujitetea kuanzia saa nne kamili asubuhi akiongozwa na wakili wake, Juma Nassoro.
Katika utetezi wake Scorpion alikanusha makosa hayo na kusema hahusiki hivyo kumuomba hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Flora Haule, amuachie huru.
Katika utetezi huo Scorpion aliiambia mahakama hiyo kuwa:
Siku ya tukio Septemba 6 mwaka jana nikiwa mlinzi wa wafanyabiashara wa eneo la Buguruni kuanzia Reli ya Tazara mpaka daraja jipya karibu na kituo cha kuelekea Ubungo kwenye mida ya saa nne usiku nilisikia makelele upande wa Shell na niliposogelea nilikuta kuna kundi la watu linamshambulia mtu.
Nikiwa kwa mbali niliwasogelea madereva wa bodaboda na kuwauliza aliyekuwa akipigwa ni nani waliniambia ni kibaka. Waliponiambia hivyo mimi nilirudi kwenye baa ya Kimboka lakini nikashangaa baada ya siku mbili nikaanza kuonyeshwa mitandaoni kuwa ndiye niliyekuwa nikimpiga yule kibaka na nimemtoboa macho.
Hata hivyo nilishangaa sana na baada ya siku mbili tena niliitwa kituo cha polisi cha Buguruni na kuhojiwa kufuatia tukio hilo, nilikataa kuhojiwa bila ndugu zangu lakini polisi walinihoji kinguvu na nilipokataa waliandika maelezo yao na kunilazimisha kuyasaini.
Nilikataa lakini walinifuata polisi wawili ambao walinipiga sana na kuniambia kwa kuwa najifanya mwanaume basi watanitoa uanaume wangu, hivyo nikalazimika kuyasaini baada ya kuzidiwa.”
Akiendelea kujitetea, Scorpion alisema shahidi wa kumi wa upande wa mashitaka kwenye kesi hiyo, Salum Masoud a.k.a Jerry Anthoni, ni mmoja kati ya wahalifu aliokuwa akiwadhibiti eneo hilo, hivyo alitoa ushahidi wa kumgandamiza ili yeye aondoke eneo hilo na aendelee na uhalifu.
Scorpion alisema kuwa shahidi huyo aliwahi kufungwa miaka mitano katika gereza la Keko, jambo linaloonesha kuwa shahidi huyo ni miongoni mwa wahalifu aliokuwa akiwadhibiti hivyo wanalipa kisasi.
Akiendelea kujitetea, Scorpion alimwambia hakimu kuwa katika maisha yake hajawahi kushitakiwa kwa kesi ya jinai ya aina yoyote, hali inayoonesha hakuwa mtu wa matukio ya uhalifu.
Katika utetezi huo Scorpion aliukanusha ushahidi uliotolewa na majeruhi huyo kwa kutaja wajihi wa mtu aliyemfanyia ukatili huo kwa kuwa wajihi huo si wa mtu mmoja.
Mshitakiwa huyo aliiambia mahakama hiyo kuwa upande wa mashitaka ulitakiwa kuwasilisha mahakamani hapo vidhibiti kama hizo cheni mbili anazodaiwa kumpora majeruhi huyo au silaha iliyotumika kufanyia uhalifu huo.
Katika kumalizia, Scorpion alisema katika tukio shahidi muhimu aliyetakiwa kupelekwa mahakamani hapo ni yule aliyedaiwa kuwa alikuwa akimuuzia kuku majeruhi huyo na alipoitwa na kukataa akaanza kushambuliwa.
Scorpion alisema shahidi huyo ndiye angekuwa muhimu upande wa mashitaka lakini kwa sababu wanazozijua wenyewe hawakuamua kumpeleka mahakamani hapo.
Baada ya utetezi huo, akiongozwa na wakili wake, ulifikia wakati wa wakili wa upande wa mashitaka, Nassoro Katuga, kuanza kumbana maswali lakini wakili wa Scorpion aliomba mahakama iahirishe kesi mpaka jioni akasimamie kesi nyingine Mahakama Kuu na muda ukizidi wakubaliane siku nyingine ya kusikiliza kesi hiyo.
Mpaka tunaelekea mitamboni tarehe nyingine ya kusikilizwa kesi hiyo ilikuwa haijajulikana na wakili wa Scorpion bado alikuwa Mahakama Kuu.

Post a Comment

 
Top