Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Emmerson-Mnangagwa.
ALIYEKUWA makamu wa Mugabe, Emmerson Mnangagwa alifukuzwa kazi mapema mwezi huu baada ya kutuhumiwa kwa kutokuwa mwaminifu na utovu wa nidhamu. Suala hilo lilichukuliwa kama njia ya kumuwezesha mke wa Mugabe, Grace Mugabe kuwa mrithi wa kiti cha urais. Inaripotiwa kuwa Mnangagwa alikimbilia nchi jirani ya Afrika Kusini, akihofia usalama wa maisha yake.
Hatua ya kumfukuza Mnangagwa ilikuwa ni kosa kubwa lililofanywa na Mugabe na sasa inaonekana kuwa makamu huyo wa zamani wa rais anayejulikana kama ”Mamba,” atarejea Zimbabwe kama mshindi.
Wakati huo huo, China imesema inauheshimu uamuzi wa Mugabe na imeahidi kuendeleza uhusiano wake wa kirafiki. China imekuwa mshirika mkubwa wa Zimbabwe kisiasa na kiuchumi kwa miaka kadhaa, baada ya mataifa ya Magharibi kumtenga Mugabe kwa tuhuma za kukiuka haki za binaadamu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lu Kang amesema kuwa nchi hiyo ina furaha kuona Zimbabwe imetatua matatizo yake kwa amani na ufanisi na kwamba sera yake kuelekea nchi hiyo haitobadilika. China imesema Mugabe amechangia kwa kiasi kikubwa katika historia ya Zimbabwe na katika harakati za ukombozi na kupata uhuru.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, amesema hatua ya Mugabe kujiuzulu inatoa fursa ya kuandaa njia mpya iliyo huru bila ya kuwepo ukandamizaji uliofanywa na utawala wa Mugabe.
Kwa upande wake, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini ametoa wito wa kuwepo suluhisho ambalo litaheshimu matarajio ya wananchi wa Zimbabwe kwa ajili ya ustawi wa baadae na demokrasia. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani, imekiita kitendo hicho kuwa cha kihistoria kwa watu wa Zimbabwe, kukomesha nchi hiyo kutengwa na kwamba mustakabali wa nchi hiyo unapaswa kuamuliwa na watu wake.

Post a Comment

 
Top