Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
 
 Mke wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Alicia Magabe amesema amewasamehe watu waliofanya shambulio la kumpiga risasi Mume wake ingawa bado anataka haki itendeke ikiwa ni pamoja na kufahamu walifanya kwa lengo gani na nani amewaagiza.

Bi. Magabe ameyazungumza akiwa Nairobi kwenye mahojiano maalumu na gazeti la hapa nchini ambapo amesema kwamba “Binafsi nimewasamehe kwa kitu walichokifanya, lakini hiyo haina maana kwamba nisingependa kuona haki inatendeka,” alisema wakili huyo.
Ameongeza “Sitaki kuwe na mkanganyiko baina ya kusamehe na hali ya kutamani kuona haki inatendeka. Tukio hilo limemfanya nianze kuamini kuwa kuna watu walitaka kumuua Lissu, lakini hawajafanikiwa na naaamini watu hao wapo, hivyo nahofia usalama wa familia yangu".
Hata hivyo mwanamama huyo amesema kwamba mpaka sasa hajasikia kama uchunguzi wowote umefanyika au waliohussika na tukio wamekamatwa hali inayopmfanya yeye kuwazia usalama wa mumewe pamoja na yeye kama mke kwani hafahamu watu hao kwa sasa wanawaza nini.
Lissu akiwa na Mke wake Hospitali (Nairobi alipolazwa)
Akizungumzia hali ya mume wake tangu alipopata matatizo Bi Magabe amesema kwamba baada ya Lisu kupata fahamu sawasawa ari yake ipo juu sana na wala hana unyonge wala uwoga juu ya yale yaliyomtokea huko nyuma.
"Si mtu wa kusema kuwa baada ya tukio amekuwa mnyonge, mwoga au ujasiri wake umepungua. Sijawahi kupata hata kauli yake moja inayoashiria kwamba sasa atarudi nyuma. Kama mke nataka mume wangu apone, tutoke hospitali turudi nyumbani. Lakini wanapokuja viongozi wenzake kutoka Tanzania, wastaafu na wa sasa na hata hapa Kenya, kauli zake zote zinaashiria amekua zaidi kisiasa." Wakili Magabe.
Ameongeza “Anasema ‘kuna siku nitapona na nitaendelea na kazi zangu’ ili kuwatia moyo wanasiasa na wanaharakati".
Lissu alipigwa risasi Septemba 07 mwaka huu akiwa mkoani Dodoma maeneo ya nyumbani kwake Area D na watu wasijulikana na baadaye alipelekwa Jijini Nairobi, Kenya kwa ajili ya matibabu zaidi.

Post a Comment

 
Top