Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Habinder Sethi.
MSHTAKIWA Habinder Sethi ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa bado hajatibiwa. Sethiamesema hayo mahakamani baada ya wakili wake kuomba aulizwe kama ametibiwa na hakimu kumuuliza jambo lililomnyanyua Sethi ambaye alisema hajatibiwa.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema ni wazi amri ya mahakama ni lazima ifuatwe.
“Hatuwezi kila siku kuongea kitu kimoja, mahakama nilisema apelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutibiwa kutokana na matatizo yaliyoelezwa mahakamani kuwa ana puto tumboni,” amesema Hakimu Shaidi.
Amesema mahakama iliona ni busara apelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akatibiwe kwa sababu kuna wataalam.
“Matakwa yetu ni kuona mshtakiwa anakuwa na afya njema na anahudhuria kesi yake, na kwa upande wa serikali kesi hiyo inathibitika. Hainifurahishi kila siku kuongea hiki kitu, apelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akatibiwe,” amesema Hakimu Shaidi.
Hakimu Shaidi ameeleza hayo leo Alhamisi mara baada ya Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kudai kesi ilipangwa kutajwa, upelelezi wake bado haujakamilika na akaomba ipangiwe tarehe nyingine.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, wakili wa Sethi, Melchisedeck Lutema aliomba upande wa mashtaka uieleze mahakama kwa nini Seth hapelekwi hospitali. Pia aliomba mahakama itumie busara na mamlaka yake kuhakikisha Seth anapelekwa hospitali.
Kwa upande wa wakili mwingine wa upande wa utetezi, Paschal Kamala amesema washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017 na kwamba hadi leo ni siku 87, wapo rumande wanakabiliwa na mashtaka yasiyo na dhamana na maelezo ni kuwa upelelezi bado haujakamilika. Kesi imeahirishwa hadi Septemba 29, 2017.

Post a Comment

 
Top