Menu

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This


MWAKA 2002, kwenye Tamasha la Rap City jijini New York, Marekani, lilitokea tukio lililowashangaza wengi katika tasnia ya muziki baada ya rapa machachari, Dwayne Michael Carter Jr. ‘Lil Wayne’ kupigwa busu la mdomoni na mwanaume mwenzake ambaye pia alikuwa bosi wake, Bryan ‘Birdman’ Williams.Muda mfupi baadaye, wakiwa kwenye mahojiano ya kipindi cha runinga, BET’s 106 & Park, Birdman, akambusu tena Lil Wayne na kuamsha mjadala mkubwa miongoni mwa wapenzi wa muziki, hasa wa Hip Hop ambapo walianza kuwahusisa wawili hao na mapenzi ya jinsia moja.
Baadaye, Birdman alitoa ufafanuzi kuhusu matukio hayo na kidogoakapunguza kelele.“That’s my son. If he was right here, I’d kiss him again. I kiss my daughter. I kiss my other son. If you got a child, you understand. I’ll kill for him… and die for him.”
Wasanii wa Cash Money.
(Ni mwanangu. Hata angekuwepo hapa ningembusu tena. Huwa namkisi binti yangu. Huwa nawabusu wanangu wengine. Kama una mtoto, utakuwa unanielewa. Nipo tayari kuua mtu… na nipo tayari kufa kwa ajili yake).
Miaka 14 baadaye, Lil Wayne na Birdman wakiwa tayari wameshazinguana
wingu kubwa la bifu likiwa limetanda kati yao, msafara wa Lil Wayne, akiwa na wasanii wenzake, wakiwa kwenye ziara ya kimuziki pande za Atlanta, Marekani, basi walilopanda lilishambuliwa kwa mvua ya risasi, baadaye ikaja kubainika kwamba shambulio hilo liliandaliwa na Birdman na kutekelezwa na rafiki yake, ambaye pia amewahi kuwa meneja wa Young Thug.
Mtu yuleyule aliyeahidi kwamba yupo tayari kuua na kufa kwa ajili ya Lil Wayne, anageuka na kutaka kuwa muuaji wa Lil Wayne. Nini kilitokea? Kwa taarifa yako, Lil Wayne na Birdman, mastaa ambao walizoeleka kuonekana kama baba na mwanaye, wakibebana kila wanakokwenda, wamegeuka kuwa paka na chui!
Picha haziendi na hivi karibuni Lil Wayne kwa mara nyingine amesikika akimvurumishia Birdman matusi ya nguoni akiwa jukwaani kwenye shoo jijini New York.
Bifu lao limeanzia mbali lakini kihistoria, Birdman ndiye aliyemkuza Lil Wayne, tangu akiwa na umri wa miaka 9. Ni yeye ndiye aliyemfanya akawa Lil Wayne huyu ambaye dunia nzima inamtambua, amekaa naye miaka chungu nzima na ndiyo maana baada ya wawili hao kubusiana, Birdman aliposema Lil Wayne ni kama mwanaye, wanaowajua waliwaelewa haraka.
Hata hivyo, pesa imejenga uhasama mkubwa kati yao. Lil Wayne amenukuliwa akisema kuwa chini ya Birdman, ilikuwa sawa na kuishi kwenye bustani nzuri yenye kila kitu lakini ndani yake ikiwa na nyoka wengi.
Albamu ya Lil Wayne, Carter V ndiyo iliyoibua uhasama huu wa kufa mtu, hii ni baada ya Lil Wayne kulalamika
kwamba Birdman alikuwa akiikwamisha albamu hiyo kwa makusudi, ‘nongwa’ ikaanzia hapo, akalalamika kwamba Birdman amekuwa akijipatia utajiri mkubwa kwa kumnyonya Lil Wayne na wenzake, mpasuko mkubwa ukafuatia ambapo msanii huyo alipotangaza kujitoa kwenye lebo hiyo, aliondoka na wasanii wenye nguvu waliokuwa wakiipa heshima Young Money Cash Money Billionaires (YMCMB).
Kwa taarifa yako, YMCMB ilikuwa ni muunganiko wa makundi mawili, Young Money Entertainment lililokuwa chini ya Lil Wayne Cash Money Entertainment la Birdman.
Kwa hiyo baada ya kujitoa YMCB, Lil Wayne akabaki na wasanii wake, wakiwemo Drake, Nicki Minaj, Mack Maine, Jae Millz na Cory Gunz na Bird Man akawa ‘looser’ wa vita hiyo maana ilimlazimu kuanza kuwapika upya wasanii wengine, ni hapo ndipo walipoanza kusikika akina Jay Sean, Future, Fly Rich, Stevie J, Future, Tyga, Meek Mill na Mystikal.
Wengi walitabiri kwamba kujitoa kwa Lil Wayne YMCMB huo ungekuwa mwisho wake pamoja na wote alioondoka nao kwa sababu tangu akiwa mdogo alikuwa chini ya uangalizi wa Birdman, leo atawezaje kusimama peke yake?
Hata hivyo, mpaka sasa upepo unaonesha kwamba Lil Wayne na wenzake wanazidi kushaini na bado wanazidi kujiimarisha,
tazama mafanikio aliyonayo Drake na Nick Minaj! Katika kila pesa wanayoingiza, Lil Wayne ana shea yake, kuanzia shoo mpaka mauzo ya albamu.Hata hivyo, kujitoa kwake YMCB hakukumaanisha mwisho wa vita, Januari 2015, Lil Wayne alifungua kesi ya madai, akitaka kulipwa dola milioni 51 na Birdman kwa kuchelewesha albamu yake na kumtumia kwa kipindi chote tangu alipokuwa msanii chipukizi mpaka sasa.Ni uhasama ambao umefikia hatua ya pande mbili hizo kuanza kuwindana kwa kutumia Uzi (bunduki za Kiisrael). Mara kadhaa wamewahi kuonekana pamoja, baadaye wakatangaza kumaliza bifu lakini inaonesha ni kama hakuna ambaye yupo tayari kumuona mwenzake akiendelea kupumua.
Urafiki na undugu wao, uliwapatia pesa, pesa zikawagawanya na kuibua visasi na sasa, wanawindana kama paka na panya. Tuombe yasitokee kama ya Notorious BIG na Tupak Shakur.

Na Hashim Aziz kwa msaada wa mitandao, Uwazi

Post a Comment

 
Top